Watalaamu wa Misitu SUA watakiwa kuhamasisha utunzaji wa misitu

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima amewataka Wataalamu wa Misitu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuhamasisha utekelezaji wa utunzaji na uendelezaji wa misitu nchini kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Amebainisha hayo Oktoba 3, 2024 wakati wa kufunga Maadhimisho ya Miaka 50 ya kuanzishwa kwa Kitivo cha Mafunzo ya Misitu kilichopo SUA ambapo amesema kitu wanachotakiwa kukifanya ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuisadia  kupata uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa Misitu katika maeneo yote kwa ajili ya kukiwezesha kizazi kijacho kuja kunufaika na misitu na mazingira kiujumla.

Aidha Malima amesema Wataalamu kutoka SUA wanapaswa kuifahamisha jamii athari zinazotokea kutokana na uharibifu wa misitu ambao kwa kiasi kikubwa unasababishwa na shughuli za binadamu ikiwemo kuchoma mkaa, kukata kuni na shughuli za kilimo hasa maeneo ya pembezoni mwa miji.

Kwa upande wake Bi. Metrida Kaijage Mtaalamu wa Sheria  kutoka SUA amesema wataalamu wana wajibu wa kutunga miswada na kupeleka kwa Serikali ili kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali misitu lakini pia amezitaka Taasisi kama SUA kutafuta wadau ambao watashirikiana nao katika uratibu wa uhifadhi misitu.

“Natumaini ni yangu  kutoka kwa wataalamu  kutoka SUA mtaendelea kufanya tafiti zenye tija kuhusiana na misitu ikiwemo njia sahihi za kutatua changamoto za kidunia ambazo zinaathiri misitu na mazao yake pamoja na tafiti za kisayansi za misitu”, amesema Bi. Metrida Kaijage.

Naye Prof. August Temu ambaye pia ni Mtaalamu mbobevu wa Misitu kutoka SUA amesema anaiona Tanzania ikiendelea kufanya vizuri katika utunzaji wa Misitu kwani SUA inaendelea kuzalisha wataalam wengi wa misitu ambao watazidi kuwa vinara wa utunzaji Misitu na rasilimali zake kwa manufaa makubwa ya jamii na kizazi cha kesho.

“Miaka 50 ijayo naiona Tanzania ikifikia hatua ya nchi kama Finland na China ambazo zinatumia vizuri mazao ya misitu kwani katika nchi hizo kila zao la msitu lina matumizi katika viwanda vya  uzalishaji malighafi, ambazo zinatumika kuinua uchumi wa nchi hivvo naamini Tanzania itafikia hatua hiyo kama endapo tu watu wataweza kutunza misitu kikamilifu”, amesema Prof. Temu

Kwaa upande wake Agnes Sirima ambae ni Rasi wa ndaki ya Misitu Wanyamapori na     Utalii, amesema ndaki hiyo imedhamiria    kuendeleza kituo cha umahiri katika taaluma ya misitu ambacho kipo chini ya SUA chenye lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusiana na Misitu lakini pia kwa ajili ya kujiendeleza kwa Wafanyakazi ambao wapo katika sekta ya Misitu.

Aidha ameongeza kuwa wanatarajia kuongeza ushirikiano kati ya SUA na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Taasisi zake zote ili kuendeleza taaluma ya misitu nchini lakini pia kuongeza wigo mpana wa mafunzo kwa vitendo kwa Wanafunzi pamoja na kuhakikisha tafiti zinazofanywa SUA zinaifikia jamii na kuboresha sera za uendeshaji sekta ya misitu nchini. Makala hii imeandaliwa na Eden Bahati, SUA TV Media.

 

Global Biodiversity Information Facility

Related Posts