Mwongozo wa uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu ya asili

Tanzania ina eneo la kilomita za mraba 94,500 sawa na hekta milioni 94.5. Kati ya hizo, takriban hekta milioni 481 ni misitu na misitu matajiwazi. Kati ya hekta milioni 48., hekta milioni 28.0 ni hifadhi ya maji, ardhi na bioanuai. Hekta milioni 20 zilizobaki ni misitu na matajiwazi ambayo uvunaji unaruhusiwa kisheria. Misitu hii inajumuisha misitu iliyohifadhiwa kwa ajili ya uvunaji na iliyopo kwenye maeneo ambayo hayajahifadhiwa kisheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Sura 323 ya mwaka 2002 hairuhusiwi kuvuna miti katika misitu ya hifadhi ya vyanzo vya maji, ardhioevu na bioanuwai.

Rasilimali ya misitu ina umuhimu mkubwa katika suala la uhifadhi wa mazingira na inakadiriwa kuchangia asilimia 2 hadi 3 kwenye pato la Taifa. Aidha, shughuli mbalimbali zinazofanywa katika maeneo ya misitu huchangia kupunguza umaskini miongoni mwa jamii ya Watanzania. Misitu pia ni chanzo muhimu cha nishati kwa kuwa asilimia 95 ya nishati nchini hutokana na mimea.

Pamoja na umuhimu wake katika kuchangia pato la taifa na uhifadhi wa mazingira, baadhi ya misitu iliyohifadhiwa na isiyohifadhiwa inaendelea kuvamiwa kwa ajili ya kilimo, malisho ya mifugo, makazi, uvunaji holela wa mazao mbalimbali, uchimbaji madini usiojali hifadhi ya mazingira na uchomaji moto. Kasi kubwa ya uvunaji wa miti kwa ajili ya magogo, mbao, nguzo na mkaa katika mikoa mingi nchini, inaashiria uharibifu mkubwa wa mazingira na kupotea na kupungua thamani kwa rasilimali ya misitu, hivyo kupoteza faida zitokanazo na kuwepo kwa rasilimali hiyo. Takwimu zinaonyesha kuwa ongezeko la ujazo wa miti kwa mwaka katika misitu yote ni meta za ujazo milioni 84, ambazo ndizo zinazoruhusiwa kuvunwa kutoka misitu ya uzalishaji. Matumizi ya miti katika mwaka 2013 yalikadiriwa kufikia meta za ujazo milioni 103.5, hivyo kuwa na upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5. Upungufu huu wa mahitaji au uvunaji wa ziadi ya kinachoruhusiwa kuvunwa kwa mwaka ni kichochezi cha uharibifu katika misitu iliyohifadhiwa.

Sera ya Taifa ya Misitu inatekelezwa kupitia Sheria na Programu ya Taifa ya Misitu ambazo zina madhumuni ya kuendeleza, kumiliki kisheria na kuwa na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa kushirikisha wadau mbalimbali. Pia Miongozo, Kanuni, Matangazo ya Serikali na Maagizo ya Kiutawala huandaliwa au hufanyiwa mapitio na kusambazwa katika nyakati mbalimbali ili kufafanua utekelezaji wa Sheria na Programu ya Taifa ya Misitu katika kuhifadhi na kusimamia rasilimali za misitu kwa ufanisi na ufasaha zaidi. Kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zilijitokeza kwenye shughuli za uvunaji na biashara ya mazao ya misitu, Wizara ya Maliasili na Utalii ilidhibiti uvunaji wa baadhi ya miti au baadhi ya mazao ya misitu katika vipindi tofauti kwenye miaka kati ya 1995 na 2000 kwa lengo la kutathmini rasilimali iliyopo. Vile vile kutokana na tathmini hizo, Mwongozo wa Uvunaji endelevu na Biashara ya Mazao ya Misitu wa kwanza uliandaliwa mwaka 2007.

Mapitio ya mwongozo wa 2007 yamefanyika ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. Utaratibu madhubuti utakaofuatwa umewekwa katika uvunaji na biashara ya mazao ya misitu na kuainisha mikakati ya kuimarisha usimamizi wa rasilimali ya misitu ya asili ili kudhibiti uvunaji usio endelevu.

Wananchi na wadau wote kwa jumla wanatakiwa kutoa ushirikiano wa dhati ili kufanikisha utekelezaji wa mwongozo huu ambao umetolewa kwa madhumuni ya kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali zetu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Mwongozo wa uvunaji endelevu na biashara ya mazao ya misitu yanayovunwa katika misitu ya asili

Global Biodiversity Information Facility

Related Posts