Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) umeanzishwa kisheria (chini ya Sheria ya Misitu Sura 323), kama chanzo endelevu cha fedha kwa ajili ya kuwezesha uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali misitu hapa nchini. Mfuko huu upo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii na unasimamiwa na Bodi ya Wadhamini. Mfuko wa Misitu Tanzania ulianza rasmi utekelezaji wa majukumu yake mwezi Julai 2011 na unafanya kazi katika Mikoa ya Tanzania Bara.
Majukumu ya Mfuko wa Misitu Tanzania yameainishwa katika kifungu cha 80 cha Sheria ya Misitu Sura 323 kama ifuatavyo:
(i). Kuwezesha uhamasishaji Jamii kupitia elimu na mafunzo kuhusu umuhimu wa
uhifadhi, uendelezaji na matumizi endelevu ya rasilimali misitu;
(ii). Kuwezesha na kugharamia uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa misitu kwa kutoa ruzuku kwa vikundi na wadau wengine wanaojihusisha na uhifadhi, usimamizi na uendelezaji wa rasilimali misitu;
(iii). Kukuza, kuendeleza na kugharamia utafiti kwa lengo la kuboresha uhifadhi, uendelezaji na usimamizi wa rasilimali misitu;
(iv). Kusaidia na kuiwezesha Tanzania kunufaika na mipango na misaada ya Kitaifa na Kimataifa iliyopo kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda bioanuwai na kuendeleza rasilimali misitu;
(v). Kusaidia na kuwezesha vikundi na watu binafsi kushiriki katika mijadala na midahalo inayohusu misitu na kuandaa tathmini za kimazingira kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 18 cha Sheria ya Misitu Sura 323;
(vi). Kusaidia na kuwezesha vikundi na watu binafsi ili wafuate Sheria ya Misitu, kanuni na miongozo husika; na
(vii). Kugharamia shughuli nyingine zinazoendana na majukumu ya Mfuko na shughuli zinazohusiana na madhumuni ya Sheria ya Misitu Sura 323.
Mfuko wa Misitu Tanzania unashirikisha wadau katika kutekeleza majukumu yake ambapo utoaji wa ruzuku ni njia mojawapo ya ushirikishwaji. Kupitia tangazo hili, wadau wote wenye sifa wanaalikwa kuwasilisha maandiko kwa ajili ya kuomba ruzuku. Aidha, kwa mwaka 2022, kutakuwa na dirisha moja tu la kupokea maandiko kwa ajili ya kuomba ruzuku ndogo, ruzuku ya kati na ruzuku kubwa, ambapo mwisho wa kupokea maandiko ya miradi ni tarehe 31 Machi, 2022.
Kwa maelezo zaidi ya maandiko yote ya miradi, pakua kiambatisho hapa chini.
Tangazo la kuitisha maandiko kwa ajili ya kuomba ruzuku la mwaka 2022