Wataalamu na taasisi zinazohusika na utoaji wa taaluma na utafiti wa miti wametakiwa kuishawishi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzisha stoo ya mbegu ya miti ya asili ya muda mrefu ili kuepuka kuendelea kupoteza miti hiyo kutokana na uharibifu mkubwa katika misitu ya asili.
Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa kwenye mjadala katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya kuanzishwa kwa Kitivo cha Mafunzo ya Misitu katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja sehemu ya Biolojia ya Mbegu za Miti kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Fandey Mashimba amesema kwa sasa kasi ya uharibifu wa misitu na miti ya asili ni kubwa hivyo ipo haja ya wadau kutoa ushawishi kwa mamlaka ili kutengenezwa stoo itakayosaidia kutunza mbegu hizo.
“Ni dhahiri kuwa kila kukicha misitu ya asili inazidi kuteketea kutokana na shughuli za kibinadamu ambapo mti kama mvule, mninga pamoja na mpingo inaendelea kupotea bila taifa kuhifadhi mbegu zake” amesema Mashimba.
Aidha amesema ipo haja ya watoa maamuzi na watunga sheria kutumia wataalamu wa misitu katika kutoa maamuzi na kutunga sheria zinazolenga kulinda na kuhifadhi misitu ili weweze kuwashauri ipasavyo juu ya masuala yote yanayohusu sekta ya misitu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mstaafu wa Misitu na Nyuki Dkt. Felician Kilahama akitoa uzoefu wake kwenye sekta ya misitu amesema hakuna namna yoyote ya kufanya endapo wataalamu hawatasikilizwa na kuthamini michango yao katika kudhibiti na kukabiliana na uharibifu wa misiti unaosababisha mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Kilahama amesisitiza kuwa misitu ya asili ni misitu wezeshi kwenye sekta nyingine na kwamba baadhi ya mambo mengi yanayohusu misitu yanakwama kutokana na mifumo iliyopo nchini hasa kwenye utashi wa kisiasa.
Andiko hili limeandaliwa na Winfrida Nicolaus, SUA TV.