Na Halima Katala Mbozi
Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA) kwa kutambua na kuthamini mchango ambao ameutoa katika kipindi cha uongozi wake aliyekuwa Makamu wa Mkuu wa Chuo Prof. Gerald Monela wamemzawadia Ngao ya shukrani kwa ajili ya kumpongeza.
Akizungumza katika hafla fupi iliyoandaliwa chuoni hapo Rasi wa ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Prof. John Kessy amesema dhumuni la kuandaa hafla hiyo ni kumpongeza na kumkabidhi Ngao ya shukrani kwa kipindi chote cha miaka 10 alichoongoza akiwa Makamu wa Mkuu wa Chuo (SUA).
Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Prof. John Kessy akimkabidhi Tuzo ya shukrani aliyekuwa Mkamu wa Mkuu wa Chuo SUA Prof. Gerald Monela, kulia ni Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho upande Taaluma Prof. Peter Gillah.( Picha na Halima Katala Mbozi )
Prof. Kessy amesema kuwa wao kama Ndaki wameamua kumkabidhi zawadi hiyo ikiwa ni ishara ya kumpongeza na iwe kumbukumbu kwake ya shukrani kwa kile alichokifanya kipindi chote cha uongozi wake.
Kwa upande wake Prof. Gerald Monela ametoa shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi wote wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii kwa ushirikiano wao waliouonesha kwake katika kipindi chote alichokuwa nao na kuwashukuru kwa kuendelea kushirikiana nae katika shida na raha alizopitia na kuwaomba waendelee na moyo huo.
Gerald Monela akitoa neno la shukrani baada ya kukabidhiwa Tuzo ya shukrani baada ya kumaliza Uongozi wake, kutoka kulia ni Naibu Makamu mkuu wa Chuo upande wa Taaluma na kutoka kushoto ni Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyamapori na Utalii Prof. John Kessy (Picha na Halima Katala Mbozi)
Aidha Prof. Monela amewataka waadhiri wote ambao ni wazoefu kuwasaidia wale ambao hawana uzoefu wa kutosha ndani na nje ya Ndaki zote za chuo ili kuongeza ujuzi na maarifa katika utendaji na ubunifu wa Teknolojia mpya.