Wanafunzi wa mwaka wa kwanza hadi wa tatu wanaosoma Shahada ya Utalii katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wamepanda mlima Uluguru hadi katika eneo la Morning Site linalomilikiwa na Chuo hicho kwa lengo la kufanya mazoezi kwa vitendo na kujifunza mbinu za kuongoza watalii kwenye maeneo ya milima.
Akiongea na SUAMEDIA Mkuu wa Idara ya Utalii na Mapumziko uishi Dkt. Agnes Sirima amesema kuwa idara hiyo imekuwa ikiwafundisha wanafunzi hao nadharia lakini pia huwawezesha kwenda katika maeneo ya kitalii ya aina mbalimbali kwa lengo la kupata uzoefu wa kutosha kabla hawajamaliza masomo yao na kuingia kwenye soko la ajira.
“Tunaposema utalii wa kupanda kwenye milima,shughuli za utalii, uongozaji watalii na ushirikishwaji wa jamii katika utalii na vitu vingine vingi katika sekta ya utalii lazima wanafunzi wajifunze kwa matendo, hivyo tumekuja nao kuwaonyesha kituo hiki cha Morning site ili wajue kipo kwenye idara yetu na waweze kukitumia kwa ajili ya mafunzo yao ya utalii” alisema Dkt. Sirima.
Amesema hii ni mara ya pili wamekuwa wanawapelekea wanafunzi katika eneo hilo lakini mwaka huu muitikio umekuwa mkubwa tofauti na mara zingine kwani wanafunzi na waalimu wao wamejitokeza kwa wingi na anaamini zoezi hilo litakuwa endelevu ili kusaidia kuwa na wahitimu bora.
Dkt. Sirima amesema hii inawajengea wanafunzi hao ambao wanatarajiwa kuja kuongoza watalii baadae kujiamini na kujua ni vitu gani vya muhimu wanapaswa kuvizingatia kabla ya kupanda mlima na watalii ikiwa ni pamoja na kufikia malengo ya mtalii kwa kumuandaa kikamilifu kwa mavazi,viatu na vitu vingine.
Akizungumzia safari hiyo mmoja wa wanafunzi wa kozi hiyo Irene Ibrahim amesema kuwa imemjengea uwezo wa kujua changamoto za upandaji milima na kujua mambo muhimu anayopaswa kufanya kabla ya kuanza kupanda mlima peke yake au pale atakapokuwa anaongoza mtalii katika kupanda mlima.
Amesema awali hakuzingatia aina za mavazi na viatu anavyotakiwa kuvaa wakati wa kupanda mlima hali ambayo imemfanya yeye na wanafunzi wengine kupanda mlima huyo kwa tabu kutokana na viatu na mavazi waliyovaa kutokuwa sahihi.
Kwa upande wake mratibu wa safari hiyo ya mafunzo Dkt. John Ngonja amesema kuwa kuna tofauti kubwa kati SUA na vyuo vingine nchini ambavyo vinatoa kozi ya utalii kwani chuo hicho kipo karibu na asili na hivyo kutoa fursa nzuri kwa wanafunzi kufanya mazoezi kwa vitendo na hivyo kuwa bora kuliko vyuo vingine.
Amesema msisitizo wa kozi wanazozitoa ni tofauti kwani wanajitahidi kuwafundisha utalii wa asili kwahiyo hiyo ni sehemu ya kutambua asili kwa kutoa kozi za Utalii wa Wanyamapori, Masoko na utalii, Uchumi,Ukarimu na Uongozaji Watalii.